Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limekamata jumla ya watuhumiwa 153 wanaodaiwa kujihusisha na makosa mbalimbali ya uhalifu, katika misako na operesheni zinazolenga kuzuia na kudhibiti vitendo vya uhalifu mkoani humo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi , tarehe 26 Agosti 2026 amesema katika operesheni hizo wamefanikiwa kukamata wahamiaji haramu 47 katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.Wahamiaji hao wanadaiwa kuingia na kuishi nchini bila kuwa na vibali halali.
Katika operesheni hizo, Jeshi la Polisi limekamata vielelezo mbalimbali vinavyohusishwa na makosa hayo, ikiwa ni pamoja na noti bandia zenye thamani ya Shilingi 1,530,000, mirungi yenye uzito wa kilogramu 43 na bangi yenye uzito wa kilogramu 380.
Aidha, Polisi imekamata pikipiki 26, mifuko 13 ya saruji, nondo 20, mbao 70, ambapo mbao 59 zina urefu wa futi nane kila moja, pamoja na baiskeli moja na mtungi mmoja wa kuzimia moto.
Katika upande wa mafanikio ya kesi zilizofikishwa mahakamani, jumla ya washitakiwa 24 wamepatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo vya kuanzia miezi minne hadi miaka 30 kwa makosa mbalimbali.
Makosa hayo ni pamoja na wizi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ubakaji, unyanyasaji pamoja na makosa mengine.
Baadhi ya washitakiwa wamehukumiwa kulipa faini, huku wengine wakitakiwa kutumikia vifungo endapo watashindwa kulipa faini walizoamriwa na mahakama.
Katika hatua nyingine, Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga kimebaini jumla ya makosa 5,291 ya ukiukaji wa Sheria za Usalama Barabarani kupitia operesheni mbalimbali.
Kati ya makosa hayo, 4,079 yalihusu magari, huku 1,212 yakihusu bajaji na pikipiki.
Wahusika wote wamechukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kulipa faini za papo kwa papo.
Aidha, katika kipindi cha miezi mitatu, madereva sita wamefungiwa leseni zao za udereva baada ya kubainika kuendesha magari kwa mwendokasi wa kilomita 116 kwa saa.
Sambamba na operesheni hizo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia mikutano 448 iliyofanyika katika vituo vya redio, shule, vituo vya waendesha pikipiki, stendi za mabasi na minadani.
Elimu hiyo imelenga kuhamasisha jamii kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, kuimarisha ulinzi shirikishi na kuzingatia maadili ya vijana katika jamii.
Aidha, wananchi wameendelea kupewa elimu kuhusu umuhimu wa madereva wa vyombo vya moto kutii Sheria za Usalama Barabarani pamoja na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa wakati.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewashukuru wananchi kwa kuendelea kushirikiana nalo katika mapambano dhidi ya uhalifu na kudumisha amani na usalama.
Vilevile, limewakumbusha madereva na watumiaji wote wa barabara kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani wakati wote ili kuepusha ajali na kulinda maisha pamoja na mali za wananchi.