Na Elizabeth cosmas,Shinyanga
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kurejesha serikalini jumla ya Shilingi 236,069,957.63 katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026 kupitia ufuatiliaji wa makusanyo ya mapato, matumizi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo na uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu.
Akitoa taarifa hiyo leo, Novemba 13, 2026, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja, amesema mafanikio hayo ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo katika kupambana na rushwa na kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
Kati ya fedha hizo, Shilingi 75,500,500 zilipatikana baada ya TAKUKURU kufuatilia ukusanyaji wa mapato katika mji wa Old Shinyanga, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga. Katika ufuatiliaji huo, ilibainika kuwa fedha zilizokusanywa kupitia mashine za kielektroniki za POS hazikupelekwa benki kwa wakati kama inavyotakiwa na taratibu za ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Aidha, Shilingi 47,877,360 zilipatikana kupitia ufuatiliaji wa fedha za ruzuku ya pembejeo za kilimo katika msimu wa mwaka 2025/2026 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu. Ufuatiliaji huo ulihusisha vyama vya msingi vya ushirika wa mazao (AMCOS) kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanapata malipo yao stahiki.
Katika hatua nyingine, Shilingi 35,129,844.63 zilirejeshwa baada ya TAKUKURU kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kubaini madeni ya ushuru wa huduma (Service Levy) yaliyokuwa hayajalipwa kwa muda mrefu.
Katika eneo la ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma, TAKUKURU ilifuatilia mradi wa ujenzi wa miundombinu katika Zahanati ya Mwakitalyo, unaohusisha ujenzi wa jengo la upasuaji na jengo la wazazi, wenye thamani ya Shilingi milioni 250.
Kupitia ufuatiliaji huo, ilibainika kuwa kodi ya zuio (Withholding Tax) haikuwa imelipwa. Baada ya ufuatiliaji huo, Shilingi 2,692,139 zililipwa.
Vilevile, TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga ilifuatilia miradi 10 ya maendeleo katika halmashauri sita za mkoa huo, yenye thamani ya jumla ya Shilingi bilioni 27.9. Miradi hiyo inahusisha sekta za elimu, afya, barabara, huduma za jamii na utawala.
Naibu Mkuu TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Mwamba Masanja akizungumza na waandishi wa habari.
Katika eneo la uchunguzi na mashtaka, TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga ilifanikiwa kurejesha serikalini Shilingi 74,870,114 zilizohusishwa na uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa mali za umma.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, fedha hizo zilirejeshwa baada ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani na kukiri makosa yao.
Katika kipindi hicho, taasisi hiyo ilipokea malalamiko 134, ambapo 105 yalihusu tuhuma za rushwa na 29 hayakuhusu rushwa. Malalamiko yasiyohusu rushwa yalishughulikiwa kwa kutoa ushauri au kuelekezwa katika taasisi husika, huku yale yaliyohusu rushwa yakifanyiwa uchunguzi.
Kwa upande wa kesi, kesi 13 ziliendelea kusikilizwa mahakamani, kesi mpya saba zilifunguliwa na kesi saba zilitolewa hukumu. Kati ya kesi zilizotolewa hukumu, Jamhuri ilishinda katika kesi sita.
TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga imeendelea kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya rushwa na kuhamasisha ushiriki wao katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
Katika kipindi hicho, elimu ilitolewa kupitia klabu 100 za wapinga rushwa, semina 44, mikutano ya hadhara 41, maonesho 14, makala saba za habari na vipindi saba vya redio.
TAKUKURU imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kupitia utoaji wa elimu kwa umma, ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo na usimamizi wa mapato ya ndani.
Aidha, taasisi hiyo imewataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kushirikiana nayo katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa za vitendo hivyo kupitia njia rasmi za mawasiliano, ikiwemo namba ya bure 113.
“Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu; tutimize wajibu wetu.”







